Mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha
televisheni cha Channel Ten Daud Mwangosi leo amefikishwa tena katika Mahakama
ya Hakimu Mfawidhi ya Wilaya kujibu shitaka lilalomkabili huku akiwa chini ya
ulinzi mkali wa askari.
Akisomewa shitaka lake na mwendesha mashtaka wa serikali Mkuu lilian Ngilangwa, amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni askari mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23) mkazi wa FFU Iringa, anakabiliwa na shitaka la mauaji ya makusudi.
Amesema mtuhumiwa huyo mnamo 02 Septemba mwaka huu katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa anatuhumiwa kumuua Daudi Mwangosi kwa makusudi kinyume na kifungu cha sheria namba 148 kifungu kidogo 5A.i cha makosa ya jinai.
Mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa mahakama ya hakimu Mfawidhi ya Wilaya Dyness Lyimo mtuhumumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haiwezi kusikiliza kesi za mauaji.
Mtuhumiwa amerudishwa mahabusu kutokana na kesi yake kukosa dhamana kisheria na kesi hiyo imeahirishwa hadi 7 Novemba mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.
No comments:
Post a Comment