Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius ameufungua rasmi
hapa Bonn, Ujerumani, mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya
tabia nchi unaolenga kufikia mwafaka kudhibiti gesi chafu
Mkataba huo kisha utakamilishwa mjini Paris baadaye mwaka huu. Kufikia
lengo la nyuzi joto mbili limekuwa suala kuu kwa wajumbe wa mazungumzo
ya tabia nchi na wanasayansi, ambao wanasema ndicho kikomo ambacho
kupindukia kwake kutaufanya ulimwengu ukabiliwe na majanga yanayoendelea
kutokea ya mafuriko, ukame, na vimbunga.
Lakini ikiwa imesalia miezi sita kabla ya viongozi wa ulimwengu kukutana
mjini Paris, matarajio yanadidimia ya kupatikana muafaka ambao utaweka
kiwango cha wastani cha joto chini ya kikomo hicho. Uzalishaji wa gesi
chafu umefikia viwango vya juu kabisa katika miaka ya karibuni.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius ameufungua mkutano
wa Bonn wa siku kumi ambao utaendelea kutathmini mafanikio ya
kuzishughulikia mbinu mwafaka za kuimarisha atua za mabadiliko ya tabia
nchi kabla ya 2020, mwaka ambao mkataba mpya utaanza kutekelezwa.
Rasimu ya sasa ina kurasa 80 za mitazamo ya kitaifa, mingine ambayo
inaingiliana na kutoa misimamo inayotofautiana. Lengo la mkutano wa Bonn
ni kuwasilisha mkataba ambao utaokoa hali ya hewa ya ulimwengu dhidi ya
uharibifu unaotokana na joto kali linalosababishwa na gesi chafu.
Mkataba huo utazitaka nchi wanachama kuweka sheria za kudhibiti
uzalishaji wa gesi chafu na kuzisaidia nchi maskini ambazo zinakabiliwa
na kitisho cha ukame, mafuriko na kupungua kwa viwango vya maji
barahini.
Baadhi ya nchi zinataka kuweka malengo ya hatua kwa hatua na mataifa 38
pekee - ikiwemo Marekani, Umoja wa Ulaya, Urusi na Canada – yameahidi
kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. Mkataba unaotafutwa
utazifungamanisha kisheria zaidi ya nchi 190 kabla ya kuanza kutekelezwa
mwaka wa 2020.
Mkutano wa kundi la nchi saba zilizostawi kiviwanda ulimwenguni – G7,
utakaoandaliwa katika jimbo la Bavaria hapa Ujerumani mnamo Juni 7-8,
huenda pia ukayajadili mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa.
Christiana Figueres,mjumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya
tabia nchi anasema serikali zinahitaji kubadilisha mitazamo yao na
kutegemea uchumi unaotokana na kiwango cha chini cha kaboni, kwa
kuzingatia nishati safi kama vile upepo au nguvu za jua, ambazo zinaweza
kuimarisha ukuwaji uchumi, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kubuni
nafasi za kazi.
No comments:
Post a Comment