Wednesday, June 19, 2013

WATOTO WAZIDI KUTUMIKISHWA MBEYA



NA GODFREY DANIEL

UTUMIKISHWAJI  wa watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka (17) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani mbeya umezidi kushika kasi na kuhatarisha maisha na elimu ya kizazi kijacho.

Hayo yamebainika baada ya uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu wilayani humo kwa zaidi ya miezi mitano kuanzia januari hadi mei mwaka huu.

Utafiti umebaini kuwa mwezi januari hadi mei mwaka huu idadi ya watoto wanaotumikishwa na wafanyabiashara katika uuzaji wa kutembeza nyama choma maarufu kama mishkaki katika Bar mbali mbali wilayani humo ilikuwa 4-6 kwa kila dakika kumi (10) wakiingia ndani ya hizo bar wakati mwezi aprili hadi mei idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 10-15 kwa kila dakika kumi (10).

Imeelezwa kuwa hali ya kuongezeka kwa watoto hao ni kutokana na ushawishi mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara ili waweze kushawishi wenzao katika kuendeleza biashara zao na kusababisha watoto wengi kuamua kuachana na masomo na kujiunga na ujira wa shilingi elfu moja kwa siku.

Baadhi ya watoto waliohojiwa na mwandishi wa habari wamesema kuwa wamelazimika kujiingiza katika kazi hiyo licha ya kufaulu kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na mabosi wao kuwahidi fedha nyingi ili ziwasaidie katika maisha yao jambo ambalo wamesema hawatekelezewi.

Akizungumzia kuhusu ongezeko hilo la watoto Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Kyela Michael Kidago amesema kuwa hali hiyo ni hatari kwani inaweza kuhatarisha maisha ya watoto wa kizazi kijacho kutokana na wengi wao kuachana na masuala ya elimu na kulazimika kufanya kazi hiyo hadi majira ya saa saba usiku.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kyela Njau amesema kuwa tatizo la kuwepo kwa watoto wengi kunachangiwa na wazazi wenyewe ambapo amesema kuwa wamekuwa wakiwapa huru watoto kiasi cha kijiamulia masuala yao.

No comments:

Post a Comment