Wednesday, June 12, 2013

IVORY COST KUTUA LEO BILA DROGBA TORE NDANI



MSAFARA wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Tembo wa watu 80 wakiwemo wachezaji 27 unatarajiwa kuwasili nchini kesho (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars bila mshambuliaji wake mkongwe Didier Drogba anayechezea Galatasaray ya Uturuki.
Mechi hiyo itachezwa Jumapili (Juni 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 9 kamili alasiri, na itachezeshwa na Charef Mehdi Abdi kutoka Algeria.

Kikosi hicho kitawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 2.50 usiku na kitafikia hoteli ya Bahari Beach iliyoko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Timu hiyo inatarajia kuondoka saa chache baada ya mechi hiyo.
Wachezaji walioko katika kikosi hicho ni Abdoul Razak, Akpa Akpro Jean-Daniel Dave Lewis, Angoua Brou Benjamin, Arouna Kone, Aurier Serge Alain Stephane, Bamba Souleman, Barry Boubacar, Boka Etienne Arthur, Bolly Mathis Gazoa Kippersund, Bony Wilfried Guemiand, Cisse Abdoul Karim, Diarrassou Ousmane Viera na Dja Djedje Brice Florentin.
Doumbia Seydou, Gbohouo Guelassiognon Sylvain, Gosso Gosso Jean-Jacques, Kalou Salomon Armand Magloire, N’dri Koffi Christian Romaric, Sangare Badra, Serey Die Gnonzaroua Geoffroy, Sio Giovanni, Tiote Cheik Ismael, Toure Yaya Gnegneri, Traore Lacina, Ya Konan Didier, Yao Kouassi Gervais na Zokora Deguy Alain Didier.
Taifa Stars iko kambini hoteli ya Tansoma tangu iliporejea kutoka Marrakesh, Morocco ambapo leo na kesho itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 9 kamili alasiri. Ijumaa itapumzika, na itafanya mazoezi ya mwisho Jumamosi kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10 kamili.
Makocha wa timu zote mbili (Taifa Stars na Tembo) watakutana na waandishi wa habari Jumamosi (Juni 15 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF kuzungumzia jinsi walivyojiandaa kwa mechi hiyo.
Wakati huo huo; Kiingilio cha chini katika mechi hiyo itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili kabla ya mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi. Tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
Utaratibu katika mechi hiyo utakuwa kama ilivyokuwa katika mchezo wa Simba na Yanga, ambapo hayataruhusiwa kuingia uwanjani isipokuwa kwa yale yatakayokuwa na sticker maalumu kutoka TFF.

No comments:

Post a Comment