WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imehakikishia wananchi wa Zanzibar
kwamba uchaguzi wa marudio utafanyika kwa amani na kuwahimiza wajitokeze
kwa wingi kushiriki siku itakapofika.
Naibu Waziri, Hamad Yussuf Masauni alisema hayo jana bungeni
alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir (CCM).
Mbunge Tahir katika swali la nyongeza, alisema kwa kuwa Zanzibar
inajiandaa na Uchaguzi Mkuu, ni vyema serikali ikazipatia wilaya za
Magharibi A na B magari ya kwa ajili ya vituo mbalimbali vya Polisi.
Tahir ambaye alisisitiza kuwa kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar si jambo
geni kwa kuwa hata mwaka 1961 ulifutwa ukarudiwa mwaka 1963,
alisisitiza kwamba kuvipatia vituo hivyo magari, itapunguza watu alioita
‘mazombi’.
Naibu Waziri aliwahakikishia Wazanzibari kwamba Serikali itaimarisha
usalama kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kuhimiza wananchi
kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi
20, mwaka huu.
“Hapatakuwa na uvunjifu wa amani,” alisema.
Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Dimani, Tahir, Naibu Waziri
Masauni alikubaliana na mbunge huyo kwamba wilaya hizo za Magharibi A
na B hazina magari na mafuta ya kutosha kwa shughuli za Polisi.
Alisema hali hiyo ni changamoto kwa vituo vingi vya polisi nchini,
lakini akaongeza kuwa mgawo wa vitendea kazi ikiwemo magari huzingatia
jiografia ya wilaya, hali ya uhalifu na idadi ya watu wanaohudumiwa na
kituo husika na si idadi ya vituo vidogo vilivyopo katika wilaya husika.
Masauni alisema, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
inakusudia kuwasilisha bajeti mbele ya Bunge kuboresha hali ya vyombo
vya usafiri, mafuta na vilainishi kukidhi mahitaji halisi ya Polisi
nchini.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema ufumbuzi wa suala la Zanzibar
haupo kwenye Bunge, wala ofisi za mabalozi wa kigeni, bali upo ndani ya
katiba na sheria za Zanzibar.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira,
January Makamba, alisema hayo juzi bungeni mjini hapa, wakati akichangia
mpango wa maendeleo wa Taifa.
Alisema ufumbuzi wa tatizo la kisiasa la Zanzibar, haliwezi kumalizwa
ndani ya Bunge, kwenye ofisi za kibalozi wala barabarani bali upo ndani
ya Katiba. Pia alisema Muungano utaendelea kudumu na amani ya nchi
itadumu na kwamba nchi itaendelea kuwa ya amani na wananchi wataendelea
kufanya shughuli zao bila ya kubugudhiwa.
January alisema Rais John Magufuli anafanya kazi kubwa, hali
iliyosababisha aungwe mkono kila sehemu, hivyo si dhambi na wapinzani
wakimuunga mkono.
Wakati January akisema hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
George Masaju alisema suala la Zanzibar ni vyeti na Katiba inatambua
serikali mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar.
Alisema Katiba ya Zanzibar, si ya Muungano lakini Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inahusika hadi Zanzibar.
Masaju alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haipaswi
kuingilia masuala ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, isipokuwa kwa
mambo ya Muungano tu. Pia aliwataka baadhi ya wabunge kuacha tabia ya
kuhamasisha wananchi kufanya vurugu. Imeandikwa na Stella Nyemenohi na
Sifa Lubasi, Dodoma
No comments:
Post a Comment