BAADHI ya wananchi katika Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, wamelalamikia
kitendo cha baadhi ya askari wa vituo vya polisi Usinge na Kaliua,
kuomba rushwa kwa mtutu wa bunduki.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wamemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kusikiliza
kilio chao na wachukulia hatua baadhi ya askari wanaofanya
vitendo hivyo ili waweze kuishi kwa uhuru na amani.
Wananchi hao kutoka Vijiji vya Ugansa, Shela, Kombe, Maboha
na Usinge, walitoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Diwani wa Kata ya Usinge, Bw. Titus Kilomba.
Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni kwenye Kijiji cha Ugansa, ambapo
wananchi hao walidai kuwa, mbali ya kutishiwa kwa silaha ili kutyoa
rushwa pia wamekuwa wakibambikiziwa kesi na askari.
“Tunamuomba Dkt. Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said
Mwema, atusaidie kutatua mgogoro kati ya askari na wananchi ambao
umeanza kuvunja mahusiano wetu,” walisema.
Walidai kwamba askari hao wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi hususani
jamii ya wafugaji kwa kuwabambikia kesi kubwa kwa lengo la kutaka wapewe
rushwa.
Mkazi wa Kijiji hicho, Bw. Ngidingi Lusumisha (67), alidai yeye
walimbambikia fuvu la kichwa cha mtu na askari aliowataja katika mkutano
huo (majina tunayo), ambao walikwenda nyumbani kwake na kudai
wanamtilia shaka kuwa
anamiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria.
“Siku hiyo ilikuwa asubuhi, askari walikuja nyumbani kwangu
wakaniambia nipo chini ya ulinzi wakidai wan mashaka na mimi hivyo wanahitaji kufanya upekuzi.
“Wakati wakiendelea kunihoji, kuna mtu ambaye nadhani alikujana na fuvu
la kichwa cha mtu na kukiweka katika zizi langu la ngo’mbe ambapo wakati
wakiendelea kunihoji, askari mmoja alitokea zizini akiwa na kichwa fuvu
hilo na kudai nimekitoa wapi,” alisema.
Alisema askari hao walianza kumtisha na kumwambia “Wewe mzee sasa
utaozea jela maana adhabu ya kukutwa na fuvu la binadamu mahakamani ni
kunyongwa hivyo kama nina sh. milioni tano, wamuachie kwani kesi yake ni
nzito sana.
Aliongeza kuwa, kutokana na maelezo ya askari hao aliogopa sana hadi
kulazimika kuwalilia wakamshawishi awape sh. 200,000. ambazo alizito na
kuwapa.
Hata hivyo, Bw. Lusumisha alidai kumshukuru Mwenyekiti wake
wa Kijiji cha Shela, Bw. Martin Juma kwa kumshauri alifikishe suala hilo kwa Bw. Kilomba ili aweze kulifuatilia zaidi.
Kwa upande wake, Bw. Kilomba alisema, amekuwa akipokea malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi kuhusu
vitendo askari wa Kituo cha Polisi Kata ya Usinge ambao
wanadaiwa kuwanyanyasa raia na kuwalazimisha kutoa
rushwa kwa mtutu wa bunduki.
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Kombe, wilayani humo, Bw. Ikungile Mwandu,
alidai mtoto wake Bw. John Ikungile (25), alipigwa risasi na askari wa
Kituo cha Kaliua, kwa madai ya kuchunga ng'ombe katika shamba la jirani
la kusababisha hasara ya sh. milioni 150.
Alisema baada ya askari hao kufika nyumbani kwake, walimuweka mtoto wake
chini ya ulinzi, kumfunga pingu ambapo wakiwa njiani kumpeleka Kituo
cha Polisi, walimtaka anyooshe mikono juu na kumpiga risasi katika mkono
wake wa kulia.
Akizungumzia mkasa huo, Bw. Ikungile alisema “walinipiga risasi katika
mkono wa kulia, baada ya kuanguka na kutowa damu nyingi walinifungua
pingu na kukimbia wakiwa na pikipiki.
“Baba aliporudi alinipeleka polisi ili tukachukue PF3 ili niweze kwenda
kutibiwa hospitali lakini baada ya kufika kituoni hapo, waliniambia
tukienda hospitali nisiseme kuwa nimepigwa risasi
eti, niwaambie nimechomwa na kitu chenye ncha kali,” alisema.
Mkuu wa Mkoa huo, Bi. Fatuma Mwassa, alipoulizwa kuhusu
sakata hilo alikiri kupokea malalamiko hayo na kuwa, tayari amemuagiza
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Anthony Rutta ashughulikie suala hilo ili
wahusika waweze kukamatwa na kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya
kijeshi.
“Taarifa hiyo ninayo...tayari nilishamwagiza RPC awachukulie hatua askari wote wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo,” alisema.
Naye Kamanda Rutta alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo alidai kuwa, hana taarifa yoyote kuhusu hivyo kupingana maelezo
ya Bi. Mwassa ambaye alisema tayari alishampa maagizo.
“Nani kakuambia taarifa hizo...mimi sifahamu chochote kuhusu jambo hilo
ndio kwanza unanipa taarifa ngoja nizifanyie kazi” alisema Kamanda
Rutta.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo, Bw. Iddy Amme, alisema
chama hicho hakiwezi kuvumilia vitendo vya aina hiyo vinavyofanywa na
askari wanaokiuka madili ya kazi zao.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, alishituka sana na kuahidi
kulifikisha suala hilo katika uongozi wa CCM Taifa ili liweze
kushughulikiwa kikamilifu.
Katibu wa CCM wilayani Kaliua, Bw. Simon Yaawo, alipendekeza iundwe tume ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo kwa wahusika.
“Mimi nipo tayari kutoa ushahidi sehemu yoyote kama nitahitajika maana
tumechoka na matukio kama haya, mimi mwenyewe nilimuona yule kijana
aliyepigwa risasi (Ikungile).
No comments:
Post a Comment