Watu wanaoaminika kuwa ni majambazi, wamemjeruhi kwa
kumpiga risasi Mtawa wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Shobana
Synd na kumpora kiasi kikubwa cha fedha.
Habari kutoka kwa wenzake zilizothibitishwa na
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas zinasema kuwa mtawa
huyo raia wa India kutoka Shirika la Notre Dame, alishambuliwa kabla ya
kuporwa fedha hizo.
Kwa mujibu habari hizo, mtawa huyo aliyekuwa
akitoka benki, alijeruhiwa kwa risasi mbili wakati akisubiri kufunguliwa
geti la kuingia katika Shule ya Msingi Notre Dame.
Ingawa Watawa hao hawakuwa tayari kutaja kiasi cha
fedha zilizoporwa, habari zinasema ni zaidi ya Sh20 milioni
zilizochukuliwa benki kwa ajili ya malipo na shughuli mbalimbali za
shule hiyo.
Shule ya Msingi ya Notre Dame iliyoko eneo la
Njiro, jijini Arusha inamilikiwa na shirika hilo la Watawa ambao wengi
wao wana asili ya Asia ambako mtawa huyo, Shobana ndiye Mwalimu Mkuu wa
shule hiyo. “Alipigwa risasi mbili, moja kwenye mguu wa kushoto
uliovunja mfupa na nyingine ilipenya kwenye nyama za mkono wa kushoto
ambako kwa bahati haijagusa mfupa...Tunamshukuru Mungu anaendelea
vizuri,” alisema mmoja wa watawa kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Akizungumza katika wodi ya Hospitali ya Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), alikolazwa, mtawa huyo
alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa kuninusuru katika kifo...Walinirushia
risasi kadhaa wavamizi hao.
“Ninamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, si
ujanja wala uwezo wangu kuendelea kuwa hai hadi leo baada ya
mashambulizi yale ya risasi. Ninawaombea msamaha na rehema wahusika ili
waache uovu na kurejea katika njia ya haki.”
Kamanda Sabas mbali na kukiri kutokea kwa tukio
hilo alishindwa kulizungumzia kwa undani kwa maelezo kuwa muda huo
alikuwa akiendesha gari na kuahidi kulitolea ufafanuzi leo.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya wateja wanaochukua
fedha kutoka benki mjini Arusha kuvamiwa na kuporwa fedha, matukio
ambayo yanazua hisia ya kuwapo mtandao wa uhalifu unaoshirikisha baadhi
ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.
Mwaka jana, wafanyakazi wawili wa Shirika la
Here’s Life Africa Mission linalomilikiwa na Askofu wa Kanisa Anglikana
Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Hotay waliochukua fedha katika
moja ya benki hizo walivamiwa na kuporwa zaidi ya Sh10 milioni.
Tayari uongozi wa benki zilipochukuliwa fedha hizo
umeanza uchunguzi kuhusu jambo hilo kwa nia ya kubaini kwa nini taarifa
za wateja wanaochukua fedha zinafika kwa majambazi ambao huwapora
njiani
No comments:
Post a Comment