Saturday, December 22, 2012

MWAKYEMBE AWASIMAMISHA VIGOGO BANDARINI



WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewasimamisha kazi vigogo 16 wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa tuhuma za ufisadi.

Idadi hiyo inafanya waliosimamishwa kazi katika bandari hiyo hadi sasa kufikia 23.
Akizungumza na wafanyakazi wa TPA Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe alisema vigogo hao wamesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali.

“ Bodi imewasimamisha kazi kutokana na tuhuma mbalimbali za wizi na migongano ya kimaslahi, hawa wamesimamishwa baada ya bodi kuichambua ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na tume niliyoiunda,” alisema.

Waliosimamishwa kazi na nyadhifa zao kwenye mabano ni Bakari Kilo (Mkurugenzi Uhandisi), Raymond Swai (Meneja Uhandisi), Frolence Nkya (Mkurugenzi wa Mipango) na Mahebe Machibya (Meneja Ununuzi na Ugavi).

Wengine ni Teophil Kimaro (Meneja Ununuzi), Mary Mhayaya (Afisa Uhandisi Mkuu), Ayoub Kamti (Mkurugenzi wa Tehama), Mathew Antony (Meneja Kitengo cha Kontena) Maimuna Mrisho (Mkurugenzi wa Mifumo wa Menejimenti).

Wengine ni Fortunatus Sandalia (Askari kitengo cha Ulinzi), Fadhili Ngolongo (Kitengo cha Marine), Mathew Antony (Meneja Kontena), Mohamed  Abdullah (Kitengo cha Mafuta), Kilimba (Idara ya ulinzi) na Owen Rwebu.

Mwakyembe alisema katika ripoti ya uchunguzi imegundulika kwamba baadhi ya vigogo wa Bandari wanamiliki kampuni ambazo zinafanya kazi za TPA.

“Tumebaini kuwa kuna mgongano mkubwa wa kimaslahi ndani ya bandari, kuna wafanyakazi wengine wana kampuni za mkononi ambazo hazijasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) lakini zimepewa kazi za TPA,” alisema.

Alisema kampuni hizo zinapomaliza muda wa mikataba yao huongezewa muda wa mikataba mingine.
Dk Mwakyembe alisema kuna mtandao mkubwa unaofanywa kwa watu mbalimbali kwa kushirikiana na vigogo wa bandari ili kufanikisha wizi katika bandari.

“Kontena zinayeyuka, zinaibwa kama Twiga walivyopandishwa kwenye ndege, ninaapa mtandao huu nitaumaliza hapa bandarini,” alisema Mwakyembe huku akishangiliwa na wafanyakazi.
Aidha Mwakyembe amepiga marufuku utaratibu wa kuingia bandarini na kulipia kiingilio cha Sh200 unaojulikana kama potipasi.

“ Utaratibu huo ndiyo umekuwa ukisababisha wizi bandari, ni marufuku watu wasiohusika kuingia bandarini, Sh200 wanazotoa zitatusaidia nini,” alihoji Mwakyembe.

Hata hivyo alipongeza juhudi ambazo zimeanza kuonekana katika mamlaka hiyo ya kuongeza mapato kila mwezi tangu alipoisimamisha bodi hiyo.

Alisema mamlaka hiyo kabla ya mageuzi ilikuwa inakusanya mapato ya Sh28 bilioni lakini sasa inakusanya Sh50 bilioni kwa mwezi.

Aidha, Mwakyembe alisema watumishi wa bandari waliajiriwa kwa njia za ujanja ujanja watachunguzwa na hatimaye kufukuzwa kazi.

“Bandari tumebaini kwamba kuna wafanyakazi wengi ambao wameajiriwa kwa undugu, ujomba ujomba, tutawashughulikia katika siku chache zijazo,” alisema.

No comments:

Post a Comment